KIZUNGUZUNGU WAKATI WA UJAUZITO

Ni kawaida kwa wanawake kuhisi kizunguzungu wakati wa ujauzito, hali hii huchangiwa na mabadiliko katika mfumo wa damu ikiwemo kupungua kwa kiasi cha damu kinachoenda kwenye sehemu ya juu ya mwili, hii husababishwa na mgandamizo wa mji wa mimba kwenye mishipa ya damu iliyopo kwenye mgongo na nyonga. Hali ya kizunguzungu hutokea sana kuanzia miezi sita ya ujauzito, wakati amabapo mishipa ya damu imetanuka lakini kiwango ch damu hakijaongezeka kujaza hapo.

Hali ya kizunguzungu inaweza kutokea pia kwenye mazingira ya joto kali au ukioga kwa maji yenye moto kupita kiasi. Mwili ukipata joto sana, mishipa ya damu kwenye ngozi hutanuka na hivyo kupunguza kiwango cha damu kinachorudi kwenye moyo.

Upungufu wa sukari kwenye damu inaweza kutokea mwanzoni mwa ujauzito na huweza kusababisha kizunguzungu. Hali hii huweza kusababishwa pia na upungufu wa damu, msongo wa mawazo, uchovu na  njaa.

Kuzuia

  • Inuka taratibu unapobadilisha mkao kunyanyuka ukiwa umelala ama umeketi
  • Tembea taratibu na pumzika mara kwa mara
  • Epuka kulala chali, badala yake lala ubavu huku ukiweka mto chini ya kiuno
  • Epuka kupata joto kupita kiasi. Punguza kukaa kwenye maeneo yenye joto na watu wengi, hakikisha maji ya kuoga siyo ya moto sana, fungua milango na madirisha kuzuia chumba kupata joto kupita kiasi
  • Kula milo midogo midogo na mingi kila siku badala ya kula milo mitatu mizito
  • Fanya mazoezi kusiadia damu kutembea vizuri kwenye sehemu ya chini ya mwili
  • Kunywa vimiminika vingi haswa maji majira ya asubuhi
  • Kula vyakula vyenye wingi wa madini ya chuma kama maharage, nyama nyekundu, mboga za majani na matunda yaliyokaushwa. Tumia pia dawa za kuongeza damu kama vidonge vya kuongeza damu vinavyotolewa kliniki