Ujauzito Wiki ya 1 na ya 2

Ujauzito Wiki Ya kwanza

Wiki mbili za mwanzo kabla ya ujauzito huhesabiwa kama miongoni mwa wiki za ujauzito kwa sababu huhusisha suala la yai kukomaa na kupevushwa, baada ya siku 6 za yai kupevushwa ikiwa patakuwa na mbegu za kiume za kurutubisha basi mimba itakuwa imetunga. Unakuwa mjamzito pale yai lililokutana na mbegu ya kiume linapokuwa limetengeneza kiumbe ambacho hujishikiza kwenye mji wa mimba. Kwa hiyo wiki mbili za mwanzo tunazihesabu kama siku za mwili kujiandaa kwa ajili ya ujauzito. Na kwa sababu hiyo tunazihesabu ndani ya wiki 40 za ujauzito.

Wiki ya kwanza ni wiki ambayo yai hurutubishwa. Hiki ni kipindi ambacho yai lililokomaa na kupevuka(ovulation) kutoka kwa mwanamke, hurutubishwa katika sehemu za uzazi za mwanamke na zaigoti hutokea tayari kwa kuanza safari ya wiki 40 akiwa tumboni kwa mama. Ujauzito uliokamili na salama ni ule ambao yai la mwanamke lililokomaa na kupevuka hurutubishwa na mbegu moja ya mwanaume. Pia ni ujauzito ambao unajipandikiza katika mji wa mimba (uterasi).

Ikitokea ujauzito umejipandikiza sehemu nyingine katika via vya uzazi wa mwanamke kama vile, mirija ya falopiani, au kwenye ovari itasababisha mtoto asiweze kukua na ujauzito kuharibika. Pia ikitokea yai moja la mwanamke limerutubishwa na mbegu zaidi ya moja, basi muunganiko huu hauwezi kutengeza mtoto aliyekamilika. Mchoro hapa chini unakuonesha namna yai lililokomaa linavyopevuka kwenye ovari na baadae kurutubishwa na hatimaye kuendelea na hatua zinazofuata.

Ujauzito Wiki Ya Pili

Kuna mambo mbali mbali yanayotokea katika wiki ya pili ya ujauzito, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na: Mabadiliko ya vichocheo vya mwili homoni, Wakati wa ovulesheni kupevuka na kutoka kwenye ovari lililokomaa kichocheo cha mwili cha estrogeni huongezeka kwa kasi zaidi kwaajili ya kuandaa mwili, hasa ukuta wa mji wa mimba kupokea yai lililorutubishwa; katika kitabu hiki tutaita zaigoti. Baada ya ovulesheni kichocheo cha progesteroni huongezeka pia ili kuandaa mji wa ujauzito kupokea ujauzito (zaigoti;-yai lililorutubishwa) na pia kujenga na kuimarisha ukuta wa mji wa mimba (uterasi) ili kutunza ujauzito pindi utakapokuwa umepatikana.

 Katika kipindi hiki cha wiki ya pili ya ujauzito mji wa mimba (uterasi) huwa tayari umejitengeneza tayari kwa kupokea na kusaidia ukuaji wa yai lililorutubishwa. Kipindi hiki pia ni kipindi ambacho yai hutolewa kutokea kwenye vimifuko vya kuhifadhia mayai(foliko) kuelekea kwenye mji wa mimba, likiwa katika mirija ya falopiani ikitokea mbegu kutoka kwa mwanaume ipo tayari katika sehemu mojawapo ya sehemu za uzazi za mwanamke, yai hurutubishwa na kiumbe kiitwacho zaigoti hutokea.

Safari ya mbegu

Masaa 24 yanayofuata huhusisha urutubishaji wa yai la mwanamke lililokomaa na kupevuka. Wastani wa mbegu za kiume milioni 15 mpaka zaidi ya milioni 200 kwa kila mililita moja ya ujazo hutoka kwa mwanaume na kuingia kwa mwanamke kwa dhumuni hili muhimu kabisa la urutubishaji. Mbegu hizi huingia kupitia uke hadi kwenye mji wa mimba (uterasi) na kusafiri zaidi mpaka kuifikia mirija ya kusafirisha mayai iitwayo falopia. Hata hivyo ni mbegu mia nne tu (400) kati ya mamilioni ya mbegu zilizotolewa zinazoweza kuhimili safari hii ya masaa kumi kutoka katika uke mpaka kwenye mirija hii ya fallopian. Pia ni mbegu moja tu itakayotangulia kupenyeza ganda la nje la yai itakayorutubisha yai hilo. Mara chache inaweza kutokea mbegu mbili kurutubisha yai moja, ambapo mimba hii huharibika.

Kuungana kwa vinasaba

Katika masaa 10 mpaka 30 baada ya urutubishaji wa yai, kiini cha yai la kike na kiini cha mbegu ya kiume huungana ili kutengeneza kiumbe kiitwacho zaigoti (Huu ndio mwanzo wa mtoto). Kama mbegu ya kiume imebeba kinasaba aina ya Y basi mtoto atakaezaliwa atakuwa wa kiume (Mwenye muunganiko wa kinasaba Y kutoka kwa baba na X kutoka kwa mama), na kama mbegu ya kiume imebeba kiini aina ya X mtoto atakaezaliwa atakuwa wa kike (Mwenye muunganiko wa kinasaba X kutoka kwa baba na X kutoka kwa mama).

Upandikizwaji (implantation)

Yai huchukua siku 3 mpaka 4 kusafiri kutoka kwenye mirija ya falopia mpaka kwenye mji wa mimba, hujigawanya katika seli ndogondogo zinazofanana 100 au zaidi likiwa njiani. Likifika katika mji wa mimba linaitwa kitaalamu blastosisti. Siku moja au mbili zinazofuata linaanza kujishikiza katika kuta za mji wa mimba ambapo linaendelea kujigawanya na kukua zaidi.

Dalili za ujauzito katika wiki mbili za ujauzito

Kwanza kabisa katika kipindi ambapo yai linakuwa halijarutubishwa kuna dalili zitakazomsaidia mwanamke kujua kuwa tayari yai limekomaa na linaweza kutolewa mda wowote kutoka katika vimifuko vya kutolea mayai tayari kwa kurutubishwa.  Kujua dalili hizi ni jambo jema, kwani humsaidia mwanamke kujua ni wakati gani akutane na mwezi wake kwaajili ya tendo la ndoa kama walikuwa wanajiandaa kupata ujauzito.

Dalili zifuatazo zitamsaidia mwanamke kujua kama yai limekwishakomaa na linaweza kutolewa muda wowote tayari kwaajili ya kurutubishwa.

  1. Kutoa ute unaoteleza ukeni.

Huu ni ute unaotoka ukeni na mwanamke anaweza kuukuta katika nguo yake ya ndani. Wakati yai likiwa limekomaa na liko tayari kwaajili ya kurutubishwa, ute huu huwa mweupe kama ute wa yai na unateleza na kuvutika.

  1. Maumivu kidogo sehemu ya chini ya tumbo

Baadhi ya wanawake hupata maumivu kidogo katika sehemu ya chini ya tumbo au upande mmoja wa kiuno wakati wa kipindi hiki cha kukomaa na kupevuka kwa yai (ovulation), hii ni kwa sababu ovari zinakuwa zinatoa mayai.

  1. Kuwa na hamu ya kufanya tendo la ndoa

Wakati huu mwanamke atapata hamu kubwa ya kutaka kufanya tendo la ndoa na mwili wake hutoa harufu ambayo huvutia kwa mwanaume. Hii ipo zaidi kwa Wanyama pia.

  1. Maziwa kujaa na kuuma

Mabadiliko ya vichocheo katika mwili wakati yai limekomaa na kupevuka hufanya maziwa kujaa kidogo na kuuma.

  1. Mabadiliko ya shingo ya uzazi

Wakati yai limekomaa, shingo ya kizazi inakua laini, yenye majimaji, na inafunguka zaidi, ili kusaidia mbegu kupenya kwenda kwenye mji wa mimba na hatimaye mirija ya falopia. Mabadiliko haya kama mwanamke akijichunguza kwa kidole na kuweza kuifikia shingo ya kizazi huweza kuyashuhudia. Ingawa itabidi mwanamke ajichunguze mara kwa mara ili kuweza kugundua tofauti.

  1. Kuongezeka kwa joto la mwili

Mwanamke anaweza kutumia kipimo joto maalumu kupima joto la kawaida kila asubuhi. Siku ambayo yai limekomaa siku ya ovulesheni joto la mwili huongezeka kidogo na hubaki hivyo mpaka mwanamke atakapopata hedhi inayofuata.

MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA UJAUZITO WA WIKI MBILI

  1. Kutumia vidonge vya kuongeza vitamini

Muda huu sio mapema kuanza kutumia vidonge vya kuongeza vitamini mwilini. Mwanamke anapaswa kuhakikisha anatumia angalau microgramu 400 za vitamini aina ya folic acid kupunguza uwezekano wa kupata mtoto mwenye shida ya mgongo wazi na shida nyingine ambazo mtoto anaweza kuzaliwa nazo.

  1. Kupanga muda wa kumuona mtaalamu wa afya.

Katika kipindi hiki ni wakati mzuri wa mwanamke kufanya uchunguzi wa afya yake kwa ujumla kama hauna shida yeyote na uko tayari kwaajili ya kupokea ujauzito. Mwanamke anapaswa kuchunguza kama kuna shida yeyote ya afya ambayo huweza kuhatarisha ujauzito, kama vile kuchunguza magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu la juu au magonjwa ya kuambukiza, au kama kuna dawa ambazo mwanamke anatumia na huweza kuleta madhara kwa ujauzito, ni wakati anapaswa kumuona mtaalamu wa afya ili abadilishiwe dawa ambazo hazitaleta madhara kwa ujauzito au kama hazina ulazima wa kutumiwa basi aache kutumia.

  1. Fikiri kuhusu vipimo vya afya

Hiki ni kipindi ambacho mjamzito na mwenzi wake wanapaswa kufanya uchunguzi wa vinasaba (genetic screening) kuona kama wana vinasaba vyovyote ambavyo huweza kumuweka mtoto katika mazingira hatarishi. Mfano ugonjwa wa seli mundu, au baadhi ya kansa. Ni vizuri kufanya uchunguzi kabla ya kuona na kama inawezekana epuka kuoa mtu ambaye ana undugu hasa kwa watu wenye magonjwa kama seli mundu.

  1. Kuwa na muda wa kukutana na mwenzi wako.

Hiki ni kipindi ambacho mwanamke hupaswa kukutana na mwenzi wake kwaajili ya tendo la ndoa mara kwa mara ili kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito. Wanandoa wengi hujikuta imewachukua muda mrefu mpaka kufanikiwa kupata ujauzito kwasababu ya kutokupata muda wa kukutana mara kwa mara.